Bayern Munich walazimishwa sare ya kibabe na Arminia Bielefeld, bao sita zafungwa

Ushindi wa mechi tano mfululizo kwa vinara wa Ligi Kuu nchini Ujerumani Bundesliga Bayern Munich umefikia tamati baada ya kulazimishwa sare ya kibabe na kibonde Arminia Bielefeld, sare ya bao 3-3 katika mchezo uliopigwa dimba la Allianz Arena.

Ukiwa ni mchezo wa kwanza wa Ligi tangia wafanikiwe kutwaa taji la Kombe la Dunia ngazi ya vilabu, Bayern walijikuta wako nyuma kwa goli 2-0 kabla ya mapumziko goli zikifungwa na Michel Vlap na Amos Pieper.

Robert Lewandowski alipunguza idadi hiyo kwa kufunga goli kabla ya Christian Gebauer kupachika bao lingine kwa Arminia Bielefeld na kufanya 3-1.

Magoli ya kuondoka na alama moja kwa vinara hao, yamefungwa na Corentin Tolisso na Alphonso Davies.

Arminia Bielefeld wamefikisha alama 18 katika nafasi ya 16 kwenye mechi 20, wakati Bayern wako kileleni kwa tofauti ya alama tano kamili mechi 13 zimesalia.

Author: Bruce Amani

Sharing is caring!

0Shares