Bayern warejea mazoezini baada ya siku 24 kutokana na Corona

Wachezaji wa klabu ya Bayern Munich wamerejea mazoezini leo Jumatatu kwa mara ya kwanza tangu kusimamishwa kwa ligi ya Bundesliga kutokana na hofu ya virusi vya Corona. Ligi zote nchini Ujerumani zilisimamishwa Machi 13 mpaka leo ambapo ndiyo wachezaji watarejea mazoezini, bila shaka kuna mwanga siku za usoni wa kurejea kwa michezo.

Shirikisho la Soka nchini humo lilitoa taarifa kuwa vilabu vyote inatakiwa virejea mazoezini Aprili 5, ambapo vinara wa ligi hiyo wameanza kuwapokea wachezaji kimakundi makundi. “Mazoezi yanafanyika bila uwepo wa watazamaji au watu wa karibu zaidi ya bechi la ufundi” taarifa ya klabu ilisema.

“Ili kuendelea kupunguza kusambaa kwa ugonjwa wa Corona, mashabiki wa Fc Bayern tunawaomba waendelea kufuata maelekezo kutoka kwenye mamlaka hivyo hawatakiwi kuja uwanjani kutazama mazoezi”.

Ligi ya Bundesliga inaendelea kusitishwa mpaka angalau mwezi Aprili 30 baada ya viongozi wa klabu kukubaliana hivyo kwenye kikao kilichofanyika Jumanne ya wiki iliyopita.

Author: Bruce Amani