Bayern yaikaba Liverpool, Lyon na Barca zatoka sare

185

Labda tumezoeshwa katika misimu ya karibuni ya kandanda la Champions League kuona mechi zenye mabao mengi na kandanda la kuvutia na kusisimua. Lakini katika uwanja wa Anfield, Liverpool na Bayern Munich, katika mtanange ambao ungeweza kuzusha msisimko na hamasa kubwa katika muongo wowote kuanzia miaka ya 70 kuendelea, zilishindwa kuwapa mashabiki uhondo waliotarajia.

Sare tasa katika mechi yao ya mkondo wa kwanza wa hatua ya 16 bora ilitokana na mechi iliyopwaya na sio kwamba kuna timu iliyocheza kandanda la kuudhi, lakini bila shaka kulikuwa na hali ya timu zote kuheshimiana kiasi na matokeo yake ni kuwaacha mashabiki wakihitaji kuona kitu kingine Zaidi ya walichopewa.

Pia ilikuwa hali ya makocha wawili na timu ambazo zilifahamu fika kuhusu hatari ambayo inazikabili. Kocha wa Liverpol Jurgen Klopp alikuwa kocha katika Bundesliga na alipambana na Bayern Munich wakati wake akiwa Borussia Dortmund. Alimfahamu mpinzani wake ndani na nje.

Vile vile, kocha wa Bayern Niko Kovac anazifahamu mbinu za Klopp na hatari anayoweza kumsababishia kama angekuwa na mchezo wa wazi.

“Tuko nyumbani sasa, hiyo ni faida na tutacheza mbele ya mashabiki 75,000. Tunafahamu kama tutafungwa, lazima tushinde. Katika kiwango hiki, tofauti ndogo sana zinaweza kuamua kila kitu kwa hiyo tusubiri kuona itakavyokuwa.” Alisema Kovac.

Klopp kwa upande wake alikosoa timu yake lakini akasema ana furaha kuwa bado ana nafasi wakati watakapoelekea Allianz Arena katika wiki tatu zijazo.

“Mechi bado haijaisha. Ilibidi tujenge msingi ambao tunaweza kuutumia katika mkondo wa pili. Kwa mtazamo wa matokeo ya leo, kila kitu kiko SAWA.” Alisema Klopp

Lyon 0 – 0 Barcelona

Messi na wenzake washindwa kutamba Ufaransa

Nchini Ufaransa, Lyon ilifanikiwa kuinyamazisha safu kali ya mashambulizi ya Barcelona wakati timu hizo zilitoka sare ya 0 – 0. Lionel Messi alishindwa kuongeza kwenye idadi yake ya mabao sita mpaka sasa kwenye mashindano hayo, wakati Luis Suarez alikuwa nafasi ambayo alibaki yeye peke yake na lango wazi lakini akapiga shuti nje, zikiwa zimesalia dakika 20 mchezo kukamilika.

Barcelona ilishindwa kufunga licha ya kupiga shuti 25 ambapo ni tano tu zilizoelekezwa langoni, lakini hakuna aliyeonyesha mchezo mzuri kati ya Lionel Messi, Ousmane Dembele na Suarez.

“Tulikuja hapa na kujaribu kuwa na mchezo mzuri lakini hatukupata bao. Shuti 25 sio kitu kibao, unapaswa kufunga lakini wakati unapokuwa na makombora mengi ina maana ulicheza vyema na tulifanya hivyo.

“Tuko imara nyumbani lakini hakuna kupinga kuwa sare ya 0 – 0 ugenini ni matokeo hatari ya mkondo wa kwanza. Tutawahitaji sana mashabiki wetu Camp Nou – yeyote anaweza kupata ushindi.”

Lyon wanatumai kuwa mshambulizi wake wa Ufaransa Nabil Fekir, ambaye hakucheza mechi ya Jumanne kutokana na kutumikia adhabu ya kadi nyingi za njano, atawasaidia kupata bao la ugenini. “Tunafahamu uwezo wake, kiufundi, kutusaidia kupata bao tunalolihitaji.” Alisema kocha Bruno Genesio.

Author: Bruce Amani