Bayern yaitungua Leipzig na kubeba Kombe la DFB Pokal

Bayern Munich wamebeba kombe la Shirikisho Ujerumani – DFB Pokal ikiwa ni mara yao ya 12 kutwaa mataji mawili ya nyumbani katika msimu mmoja. Bayern waliwabwaga RB Leipzig 3 – 0 katika fainali iliyochezwa katika dimba la Olimpiki mjini Berlin.

Bayern waliweka mpira kambani kupitia kichwa safi cha Robert Lewandowski kabla ya Kingsley Coman kuutuliza mpira kwa ustadi mkubwa na kusukuma wavuni shuti kufanya mambo kuwa 2 – 0 katika kipindi cha pili. Lewandowski kisha akaongeza la tatu katika dakika za mwisho kwa kumvisha kanzu kipa Peter Gulacsi baada ya kutimka mwenyewe kutoka katikati mwa uwanja.

Leipzig, ambao walianza kwa kujiamini sana walikuwa na nafasi nzuri za kufunga lakini wakapata kizingiti mlangoni kwa jina la Manuel Neuer. Mafanikio hayo ya DFB Pokal yana maana kuwa Niko Kovac ameiongoza Bayern kutwaa mataji mawili ya nyumbani katika msimu wake wa kwanza akiwa kocha, mwaka mmoja baada ya kuwabwaga katika fainali wakati Mcroatia huyo akiwa kocha wa Eintracht Frankfurt.

Author: Bruce Amani