Bayern yashindwa kupunguza pengo dhidi ya Dortmund

55

Mabingwa watetezi Bayern Munich walibumburushwa kwa kufungwa 3-1 na Bayer Leverkusen siku ya Jumamosi na kuwaruhusu Borussia Dortmund kutanua uongozi wao kileleni mwa Bundesliga na pengo la pointi saba.

Mabao ya kipindi cha pili ya wachezaji wa Leverkusen Leon Bailey, Kevin Volland na Lucas Alario yawalipa kichapo cha nne msimu huu Bayern ambao wanashikilia nafasi ya pili wakati Dortmund wakiongeza pointi moja kwa uongozi wao licha ya kutoka sare ya 1 – 1 na Eintracht Frankfurt. Bayern sasa wana mechi 13 za kucheza na ili kuwafikia Dortmund.

“Tunapaswa kushinda kila mechi sasa,” alisema kiungo wa Bayern Joshua Kimmich. “Kama tutaacha pointi zaidi barabarani, basi hatutaweza kuziba pengo.”

Bayern walifunga bao la ufunguzi kupitia kiungo Leon Goretzka likiwa ni bao lake la nne katika mechi tatu.

Mjini Frankfurt, Dortmund ilistahili kupata pointi moja ugenini na ilikuwa kifua mbele baada ya Raphael Guerreiro kumpa pasi safi sana Marco Reus ambaye alisukuma wavuni shuti katika dakika ya 22. Reus alikuwa na nafasi nne za kufunga mabao katika kipindi cha kwanza lakini akachemsha. Hata hivyo, Frankfurt ilisawazisha kabla ya kipindi cha mapumziko wakati Luka Jovic mfungaji wa mabao mengi kwenye ligi mpaka sasa akiwa na 14, alipombwaga kipa wa Dortmund Roman Burki, na kubusu nyavu.

Borussia Monchengladbach ilisonga hadi nafasi ya pili baada ya kushinda 2-0 dhidi ya Schalke.

Christoph Kramer na Florian Neuhaus walifunga mabao ya dakika za mwisho mwisho baada ya Alexander Nubel wa Schalke kutimuliwa uwanjani baada ya dakika ya 59.

Author: Bruce Amani