Benin kuendeleza rekodi dhidi ya Senegal robo fainali?

Baada ya mapumziko ya siku moja, Kombe la Mataifa ya Afrika Afcon 2019 linaingia hatua ya robo fainali ya michuano hiyo ambapo siku ya leo Jumatano Julai 10, Benin itacheza na Simba wa Milima ya Teranga Senegal mchezo utakaofanyika dimba la 30 June majira ya saa 1 jioni.

Benin wanaingia kwenye mchezo wa leo baada ya kuistajabisha dunia kwa kuitoa timu iliyokuwa inapigiwa upatu kunyakua taji la Afcon mwaka huu Morocco kwa mikwaju ya penati baada ya sare ya 1-1 katika dakika 120.

Benin ikiwa imeweka rekodi ya kufika kwa mara ya kwanza robo fainali ya mwaka huu, mpaka sasa imecheza mechi 4 haijapoteza mchezo hata mmoja kwa maana ina sare 4 kwenye mechi 4.

Aidha, kwa upande wa Senegal wanaingia katika mtanange huo wakiwa wametoka kushinda hatua ya 16 bora fainali ya Afcon 2019 dhidi ya Uganda kwa goli 1-0, goli la mshambuliaji wa Liverpool Sadio Mane. Mshindi wa mchezo huu atakutana na Madagascar au Tunisia hatua ya nusu fainali ya mashindano hayo.

Author: Bruce Amani

Facebook Comments