Benin yaiduwaza Morocco na kutinga robo fainali

Taifa la Benin limefanikiwa kufuzu hatua ya robo fainali kwa mara ya kwanza tangu kuzaliwa kwa kwa nchi hiyo baada ya kuifunga timu ngumu ya Morocco katika hatua ya 16 bora kwa mikwaju ya penati 4-1, baada ya dakika za nyongeza kumalizika kwa sare ya 1-1, mtanange uliofanyika Simba la Al Salaam, Cairo.

Ikiwa ni michuano ya 32 Afcon 2019, Morocco ilikuwa ni miongoni mwa timu zinazopigiwa upatu ilijikuta ikipotea kupitia goli la Moise Adilehou mapema kipindi cha pili, licha ya kutawala mpira kwa asilimia kubwa katika dakika zote 120.

Goli la kusawazisha kwa Morocco lilipatikana dakika ya 76 kupitia kwa Youssef En-Nesyri.

Baada ya kumalizika dakika za nyongeza (30) Mwamuzi aliamuru kupigwa penati ambapo matuta ya Benin yamefungwa na Olivier Verdon, David Djilga, Anane Tidjani na Seibeou Mama. Wakati penati pekee ya Simba wa Milima ya Atlas Morocco ikifungwa na Oussama Idrissi huku wachezaji Sofiane Boufal na Youssef En-Nessyri wote wamekosa.

Safari ya Benin kutoka kwenye makundi ilikuwa ya kustaajabisha ikiwa ndio timu pekee iliyotoa sare mechi zote tatu, mchezo wa Morocco ukiwa ya nne kutoa sare kwenye dakika za kawaida.

Ndoto ya kocha Herve Renard imeishia njiani ya kuwa kocha wa kwanza kushinda mataji matatu ya Afcon kwa nchi tatu tofauti baada ya Zambia na Ivory Coast.

Author: Bruce Amani

Facebook Comments