Bondia afariki Ulingoni Zimbabwe

479

Bondia kijana Taurai Zimunya amefariki duniani baada ya kupigwa kwa KO katika pambano la masumbwi lisilo la kuwania taji lililofanyika mwishoni mwa wiki iliyopita.

Zimunya mwenye umri wa miaka, 24, raia wa Zimbabwe akichezea kwenye uzito wa Super Bantam, alifariki siku ya Jumatatu, baada ya kuanguka na kuzimia ulingoni siku ya jumapili jioni, huku taarifa zikisema kuwa ubongo wake ulichanganyika na damu.

Bondia huyo baada ya kuanguka na kuzimia, alipatiwa matibabu ulingoni hapo(huduma ya kwanza), lakini hali ilizidi kuwa mbaya ndipo akawahishwa Hospitali, hata hivyo hakuweza kurudisha fahamu, kabla ya Jumatatu kufikwa na umauti.

Zimunya ambaye anatoka katika kambi ya ngumi ya Legends Boxing Club, siku hiyo alikuwa akipambana na Tinashe Majoni, kutoka kambi ya ngumi ya Charles Manyuchi Academy ya bondia maarufu, Charles Manyuchi anaweka historia ya kuwa bondia wa kwanza kufariki kwenye ulingo nchini Zimbabwe.

Author: Asifiwe Mbembela