Bosi wa Schalke ajiuzulu kwa muda kutokana na kauli za kibaguzi

Mwenyekiti wa wa klabu ya soka ya Schalke 04 ya hapa Ujerumani, Clemens Tönnies, amelazimika kujiuzulu nafasi hiyo mwa muda kufuatia matamshi yake ya wiki iliyopita ambayo yamekosolewa kuwa ya kibaguzi, ingawa haionekani kuwa matamshi hayo yatamuangusha moja kwa moja. Jacob Safari na mengi zaidi katika ripoti ifuatayo.))

Katika mkutano wa siku iitwayo ya “wafanyakazi wa mikono” mjini Paderborn alipokuwa akikutana na wageni 1,600, Tönnies anaripotiwa kukosoa kuongezwa kwa kodi kwa ajili ya kupambana na mabadiliko ya tabia nchi na akapendekeza kwamba ingekuwa bora kujenga viwanda ishirini vya kuzalisha umeme kila mwaka barani Afrika.

Tönnies alinukuliwa na gazeti la Neue Westfaliche akisema na hapa nayanukuu maneno yake “viwanda hivyo vitakapojengwa basi Waafrika wataacha kukata miti na watawacha pia kutafuta watoto giza linapoingia,” mwisho wa kunukuu.

Na sasa baada ya matamshi yake kulaaniwa sana na mashabiki wa klabu ya Schalke, bodi ya klabu hiyo imetoa taarifa na kusema kwamba mwenyekiti huyo amejiuzulu kutoka kwenye wadhfa wake japo kwa miezi mitatu tu kwa kuwa imempata na hatia ya kwenda kinyume na sera zinazopinga ubaguzi za klabu hiyo. Bodi hiyo lakini imesema kwamba haioni matamshi yake hayo kuwa ya kibaguzi kwa namna yoyote ile.

Baada ya tangazo hilo mashabiki wa Schalke kupitia kwa mwakilishi wao Susanne Franke wamesema kwamba bila shaka watapinga iwapo mambo yatasalia jinsi yalivyo na uamuzi huo hautobadilishwa na hatua kali zaidi kuchukuliwa dhidi yake.

Wawakilishi wa michezo na hata wanasiasa wamemtaja Tönnies kuwa mtu ambaye hajastaarabika na matamshi yake kama yaliyopitwa na wakati. Mchezaji wa zamani wa Schalke ambaye ni raia wa Ghana Gerald Asamoah, ambaye pia ni kocha wa timu ya Schalke ya wachezaji wasiozidi umri wa miaka ishirini na tatu, ameelezea kusikitishwa kwake na matamshi hayo akiandika kwenye ukurasa wake wa mtandao wa Instagram na hapa nanukuu “nimeshtushwa, nimeghadhabishwa na nimeumia sana, amenitukana mimi na wageni wengine wote, hatuwezi kulivumilia hilo,” mwisho wa kunukuu.

Shirikisho la Soka la Ujerumani, DFB, limesema kuwa ni jambo la kushtusha na kusikitisha kuona kwamba mtu mwenye nafasi na uzoefu mkubwa kama Tönnies anatoa matamshi mabaya kama hayo kuhusu watu wa bara zima.

Lakini kocha wa Schalke, Huub Stevens, amemtetea mwenyekiti wake kwa kusema “yeyote anayemjua Tönnies, yeyote ambaye ameshafanya kazi naye kwa muda mrefu, anamfahamu kwamba anapenda watu pasipo kujali rangi ya ngozi, asili wala dini yake.”

Author: Bruce Amani

Share With Your Friends