CAF yatoa majina ya waamuzi wa mechi ya Yanga, Rivers United

Shirikisho la Kandanda barani Afrika (CAF) limetoa orodha ya waamuzi wanne kutoka Somalia watakaochezesha mechi ya kwanza ya Champions League baina ya Yanga SC na Rivers United itakayochezwa Uwanja wa Benjamin Mkapa, Septemba 12, kuanzia saa 11 jioni.

Waamuzi ambao wameteuliwa ni pamoja na Hassan Mohamed Hagi ambaye atasimama katikati na atasaidiwa na Suleiman Bashir na Ali Mohamud Mahad huku refa wa akiba akiwa ni Ahmed Hassan Ahmed wote wakitoka huko Somalia.

Kamishna wa mchezo huo atakuwa ni Lewis Madeleine kutoka Shelisheli huku Ofisa Vipimo wa Uviko-19 akipangwa Violet Michael Lupondo wa Tanzania.

Katika mchezo wa marudiano baina ya timu hizo mbili utakaochezwa Septemba 19 huko Port Harcourt, Nigeria, refa wa kati atakuwa ni Adaari Abdul Latif ambaye atasaidiwa na Waghana wenzake Paul Atimaka, Patrick Papala na Kwame Sefah atakayekuwa mezani

Sullay Kamara kutoka Sierra Leone ndiye amepangwa kuwa kamishna wa mchezo na ofisa wa vipimo vya Uviko-19 atakuwa ni Ozi Salami Onimisi wa Nigeria.

Timu itakayopata matokeo mazuri katika mechi mbili, itasonga mbele na kutinga katika hatua ya kwanza ambako itapambana na mshindi kati ya Fasil Kenema na Al Hilal.

Author: Asifiwe Mbembela

Sharing is caring!

0Shares