Callum Hudson-Odoi akutana na Rais wa Ghana akitaka kubadilisha utaifa

Rais wa Ghana Nana Akufo-Addo ametoa maagizo kwa Waziri wa Michezo Mustapha Usif wa taifa hilo kuanza mazungumzo na winga wa Chelsea Callum Hudson-Odoi kuangalia uwezekano wa kuitumikia Ghana ngazi ya taifa hilo lililopo Magharibi mwa Afrika.
Hilo linakuja baada ya mchezaji huyo kumtembelea Rais Akufo-Addo Jumatatu Juni 7. Ikumbukwe kuwa Odoi ni mzaliwa wa Ghana lakini wazazi wake wanaishi nchini England.
Ambapo baba mzazi wa Hudson-Odoi, ni mchezaji wa zamani wa timu ya taifa la Ghana na klabu ya Hearts of Oak ambaye anafahamika kwa jina la Bismark Odoi.
Mabadiliko hayo yanaweza kufanyika ingawa kutakuwa na changamoto kufuatia mchezaji huyo kuitumikia timu ya taifa ya England.
Kwa mjibu wa sheria za FIFA zinamruhusu Odoi kuhama utaifa na endapo mchezaji anayehama atakuwa amecheza chini ya mechi tatu kwenye majukumu ya timu ya awali, ambapo winga huyo amecheza mechi pungufu.
Mechi zote hizo zimetokea akiwa bado chini ya umri wa miaka 21 ambapo atahitaji kusubiri kwa miaka mitatu kabla ya kufanya maombi hayo.
Endapo hilo litafanikiwa, Odoi atakuwa nyota wa pili mwenye asili ya Afrika ambaye anahama kutoka kuiwakilisha England na kurudi katika mataifa yao ya asili baada ya winga wa Crystal Palace Wilfried Zaha kuhama na sasa anaiwakilisha Ivory Coast kwa kile alichosema ufinyu wa nafasi katika timu ya taifa ya England (Three Lions).

Author: Asifiwe Mbembela

Sharing is caring!

0Shares