Cavani aipa ushindi Uruguay mbele ya Bolivia, yatinga robo fainali

Mshambuliaji wa Uruguay Edinson Cavani ameisaidia timu yake kushinda na kufuzu kucheza hatua ya robo fainali ya mashindano ya Copa America katika ushindi wa goli 2-0 mtanange uliopigwa Ijumaa dhidi ya Bolivia.
Strika huyo anayekipiga kunako klabu ya Manchester United bao lake alilifunga akitumia vyema krosi maridhawa ya Facundo Torres dakika 11 kabla ya kumalizika kwa kandanda.
Uruguay walitangulia kujipatia bao baada ya beki wa Bolivia Jairo Quinteros kujifunga goli akishindwa kuokoa vyema krosi ya Giorgian de Arrascaeta kabla ya mapumziko.
Ushindi huo unaifanya Uruguay kushika nafasi tatu kwenye kundi A wakivuna alama nne kwenye mechi tatu.
Kocha mkongwe Oscar Tabarez wa Uruguay atamaliza michuano ya makundi siku ya Jumatatu dhidi ya Paraguay.
Bolivia, ambao wako chini zaidi katika viwango vya Fifa, watakutana na Argentina siku ya hiyo hiyo ya Jumatatu, watahitaji ushindi kama kweli watatakiwa kuweka uwezekano wa kufuzu.

Author: Bruce Amani

Sharing is caring!

0Shares