Celtic watwaa ubingwa wa 9 mfululizo wa ligi ya Scotland

Celtic imetangazwa rasmi kuwa mabingwa wapya wa ligi kuu nchini Scotland hii inafuatia msimu wa 2019/20 kufutwa kutokana na janga la virusi vya Corona.

Ubingwa huo unakuwa ubingwa wa tisa mfululizo kwa Celtic na taji la 51 la ligi kwa klabu hiyo kongwe Ulaya.

Meneja na nahodha wa zamani wa Celtic Neil Lennon ambaye aliichukua timu hiyo kutoka mikono ya Brendan Rodgers ambaye sasa ni kocha wa Leicester City amesema kuchukua mataji tisa mfululizo ni mafanikio bora zaidi katika historia ya mpira, amekusudia timu hiyo ichukue taji la 10.

Celtic wametwaa ubingwa huo kwa kigezo cha uvunaji wa pointi kwa mchezo mmoja mmoja.

“Nilipobeba taji la nane watu walikuwa wanasema kuhusu ubingwa wa 10,” alisema Lennon.

“Tulitakiwa kubeba kwanza la tisa sasa tumetimiza, tutaangalia kama tutabeba taji la 10 kama mashabiki wetu wanavyosema”.

Kikosi cha Lennon kimefikia mafanikio ya kuchukua mataji tisa kama ambavyo Jock Stein wa Celtics mwaka 1960/70 na Rangers pia imewai kutwaa mataji mara tisa mfululizo 1989/97.

Taifa la Scotland linaungana na taifa kama Ufaransa, Ubeligiji, Uholanzi, Cameroon, Congo, Kenya pamoja na mataifa mengine ambayo yamefuta ligi zao katika utaratibu tofauti tofauti kwani kuna baadhi ya mataifa wamefuta huku bingwa akipatika zingine hakuna bingwa wala kushuka daraja.

Author: Bruce Amani