Chanzo cha kifo cha Maradona ni kukosa huduma makini – Jopo la Madaktari

Jopo la Madaktari nchini Argentina limebainisha kuwa chanzo cha kifo cha lijendi Diego Maradona ni kukosa uangalifu pamoja na huduma makini kipindi anaugua.

Jopo hilo itakumbukwa liliundwa siku chache baada ya kifo cha nyota huyo wa zamani wa Argentina na pia nahodha kutokana na msukumo wa Wananchi na wadau wa kandanda wakitilia shaka madaktari na manesi waliokuwa wanahusika kumtibu kabla ya umauti kumfika.

Maradona alifariki dunia mwezi Novemba mwaka 2020 akiwa na miaka 60 nyumbani kwake Buenos Aires kutoka na mushtuko wa moyo (heart attack).

Alifanyiwa upasuaji wa ubongo mwanzoni mwa Novemba na alikuwa anatibiwa juu ya kupunguza uraibu wa matumizi ya unywaji wa pombe kupindukia.

Kifo cha Maradona ambaye alikuwa nahodha wa Argentina kwenye Kombe la Dunia mwaka 1986 wakifanikiwa kubeba taji hilo, kilipelekea huzuni, kilio na maswali mengi juu yake kabla ya kuundwa kwa Jopo la uchunguzi.

Mwezi Machi, Jopo la wataalamu 20 walianza rasmi uchunguzi wao kujua kama kifo cha mkongwe Maradona ni kifo cha kawaida au kilichagizwa na uzembe wa madaktari waliokuwa wamepewa dhamana ya kumtazama na kumpa tiba.

Kwa mjibu wa majibu ya ripoti yenye kurasa 70 iliyoachiwa Ijumaa hii, yanasema kwamba, Maradona alikuwa kwenye hali mbaya saa 12 kabla ya kifo chake, lakini alikuwa hapewi huduma za kitabibu vizuri.

Kwenye ripoti hiyo pia wamesema Maradona alikuwa anaachwa muda mwingine bila huduma ya karibu na wataalamu hao, wanafika mbali na kusema kama kungekuwa na huduma ya karibu basi hluenda angebaki salama.

Author: Asifiwe Mbembela

Sharing is caring!

0Shares