Chelsea, Arsenal kukwaruzana fainali ya Europa League

England imekuwa nchi ya kwanza kuwa na timu nne kwenye fainali mbili za mashindano ya Ulaya katika msimu mmoja baada ya Chelsea na Arsenal kutinga katika fainali ya Europa League jana usiku.

Chelsea iliifunga Eintracht Frankfurt ya Ujerumani mabao 4 – 3 kupitia mikwaju ya penalti uwanjani Stamford Bridge, baada ya kutoka sare ya 1 – 1 kwa mara nyingine tena katika nusu fainali.

Eden Hazard alifunga penalti ya ushindi baada ya mlinda mlango Kepa Arrizabalag kuokoa penalti mbili.  Arsenal iliifumua Valencia 4 – 2 huku Pierre-Emerick Aubameyang akifunga mabao matatu ili kukamilisha ushindi wa jumla ya 7-3. Fainali itachezwa mjini Baku, Azerbaijan mnamo Mei 29.

Timu za England zimetawala kandanda la Ulaya msimu huu, baada ya Liverpool na Tottenham kufuzu fainali ya Champions League.

Arsenal watahitaji kushinda mechi hiyo ili kuingia katika Ligi ya Mabingwa msimu ujao kwa sababu kuna uwezekano isimamalize katika nne bora kwenye ligi. Chelsea tayari ina uhakika wa kumaliza katika nne bora kabla ya mechi za mwisho wikiendi

Author: Bruce Amani

Share With Your Friends