Chelsea yaduwazwa na kibonde West Bromwich Albion, yachapwa 5-2

Vibonde West Bromwich Albion wameiduwaza Chelsea katika dimba lao la nyumbani Stamford Bridge baada ya kuitandika 5-2 na kufuta rekodi ya kutopoteza kwenye mechi 14 mfululizo huku Matheus Pereira na Callum Robinson wakifunga goli mbili kila mmoja.

Chelsea wakiwa pungufu baada ya mlinzi wa zamani wa Paris St-Germain Thiago Silva kutolewa uwanjani kwa kadi nyekundu kunako dakika ya 29 walijikuta wakichapwa katika namna ya kustaajabu Stamford Bridge.

Matokeo hayo yanaisogeza West Bromwich Albion nafasi ya 19 alama saba kuelekea eneo salama la 17 ambalo linashikiliwa na Newcastle United, na hata wakishuka daraja hii itabaki kuwa siku ya kumbukumbu kwao.

Magoli ya Chelsea yamefungwa na winga wa kimataifa wa Marekani Christian Pulisic kabla ya Timo Werner kuongeza bao la pili hata hivyo goli tano za West Brom zilikuwa nyingi kusalimika kipigo hicho.

Yale mabao ya The Baggies yamefungwa na Pereira raia wa Brazil aliyeingia kambani mara mbili, Callum Robinson mara mbili, na Mbaye Diagne akahitimisha siku nzuri ofisini kwa vijana wa kocha Sam Allardyce

“Nimefurahishwa na kiwango, sio tu kwa sababu ya ushindi lakini pia namna tulivyoshinda” alisema Allardyce.

Author: Asifiwe Mbembela

Sharing is caring!

0Shares