Chelsea yaiondoa Liverpool Kombe la FA, yafuata nyanyo za Arsenal

Hali ngumu yenye majuto imeendelea kuitesa Liverpool baada ya jana Jumanne kukubali kichapo cha goli 2-0 dhidi ya Chelsea mtanange wa Kombe la FA uliopigwa dimba la Stamford Bridge.

Kichapo kinachomaanisha kuwa kikosi cha Klopp kinapokea kichapo cha pili mfululizo katika mashindano makubwa baada ya wiki iliyopita kufungwa goli 3-0 na Watford.

Chelsea, iliichapa Liverpool ambayo ilikuwa haijapoteza mechi 18 mfululizo ambayo ilikuwa na wachezaji kama Virgil van Dijk, Sadio Mane, Andy Robertson na Joe Gomez na kukata tiketi ya kucheza robo fainali ya FA.

Willian alizawadiwa goli na makosa ya mlinda mlango Adrian kufuatia kushindwa kuokoa mchomo mdogo uliokuwa umeelekezwa golini mwake kabla ya kiungo wa zamani wa Everton Ross Barkley kuipa uhakika wa ushindi Chelsea kwa goli la pili.

“Tulihitaji kiwango bora leo baada ya kupata matokeo mabaya michezo miwili iliyopita”.

“Kufunga na kuisaidia timu yangu kupata ushindi dhidi ya Liverpool ni sawa na kutimiza ndoto mimi kama shabiki wa Everton”. Alisema Ross Barkley baada ya mchezo huo.

Matokeo hayo yanaifanya Chelsea kuungana na Arsenal, Sheffield United na Newcastle United hatua ya robo fainali ya FA.

Author: Bruce Amani

Share With Your Friends