Chelsea yalala mbele ya Bayern Munich

Ndoto za Chelsea kufanya vizuri kwenye michuano ya Uefa huenda zimefikia tamati leo Jumanne baada ya kukubali kichapo cha goli 3-0 dhidi ya Bayern Munich katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya hatua ya 16 bora mkondo wa kwanza uliofanyika Stamford Bridge.

Kinara huyo wa Bundesliga amefuata nyanyo za RB Leipzig kwa kucheza na timu ya England kisha kuonyesha kandanda safi na la kuvutia, kumbuka Leipzig iliichapa Tottenham hatua kama hii siku sita nyuma

Maumivu ya Chelsea usiku huu yamechagizwa na kiwango bora alichokuwa nacho Gnabry, 24, ambaye amefunga goli 2 kwa msaada wa Robert Lewandowski huku goli la mwisho likifungwa na Lewandowski mwenyewe.

Gnabry goli za leo zinamfanya kufikisha goli sita katika michezo sita aliyocheza ya Uefa.

Katika mchezo wa marejeano Chelsea watakosa huduma ya Marcos Alonso ambaye ameonyeshwa kadi nyekundu kwa mchezo usio wa kiungwana sambamba na Jorginho ambaye ameonyeshwa pia kadi ya njano ya tatu katika msimu huu wa michuano.

Ili kusonga mbele kikosi cha Frank Lampard kinahitaji bahati na mkono wa Mungu kwani licha ya kupoteza nyumbani bado hata mchezo wao wa leo ulikuwa sio wa kuvutia, nafasi za wazi zikipotezwa mara kwa mara hivyo watahitaji kushinda angalau goli 4-0 nyumbani kwa Bayern Munich Allianz Arena.

Author: Bruce Amani

Share With Your Friends