Chelsea yamrejesha Romelu Lukaku England

Klabu ya Chelsea imekamilisha uhamisho wa mshambuliaji wa kimataifa wa Ubeligiji na Romelu Lukaku kwa dau la pauni milioni 97.6 akitokea Inter Milan.

Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 28, anarejea tena Stamford Bridge kwa mkataba wa miaka mitano baada ya kuachana na timu hiyo mwaka 2014 kwa dau la pauni milioni 24 na kujiunga na Everton.
Licha ya usajili wake kuingia kwenye sajili ghali bado usajili wa kiungo mshambuliaji wa kimataifa wa England kwenda Manchester City kutokea Aston Villa unabakia kuwa ghali zaidi pauni milioni 100.
“Nilikuja hapa kama kijana mwenye ndoto kubwa, saizi narejea nikiwa na uzoefu wa kutosha nikiwa nimekoma zaidi”, alisema Romelu Lukaku.
“Nimekuwa shabiki wa Chelsea tangia utotoni, saizi narudi kuisaidia kushinda mataji”.
Lukaku ameweka rekodi ya aina yake ambapo sasa kwa pamoja vilabu vyote ambavyo amechezea wametoa takribani pauni milioni 290 kwenye usajili wake.
Lukaku pia aliweka rekodi ya kuwa mchezaji wa tatu kwa thamani kubwa nchini Italia baada ya kuuzwa na Manchester United kwenda Inter Milan kwa dau la pauni 74 mwaka 2019.

Author: Asifiwe Mbembela

Share With Your Friends