Chelsea yashika usukani, Tammy Abraham akiipa alama tatu muhimu

Ushindi wa Chelsea wa 2 – 0 mbele ya Newcastle United umeifanya klabu hiyo kukwea mpaka nafasi ya kwanza kwenye msimamo wa Ligi Kuu nchini England wakiwa vinara kwa masaa kadhaa, unakuwa ushindi wa tano mfululizo kwa Frank Lampard katika mashindano yote.

Bao la kwanza la Chelsea lilikuwa la kujifunga la mlinzi wa kimataifa wa Argentina Federico Fernandez akijaribu kuokoa hatari ya mpira wa Ben Chilwell.

The Blues walipata uhakika wa ushindi ungwe ya pili kufuatia strika wa England Tammy Abraham kumalizia pasi sukari ya fowadi wa Kijerumani Timo Werner kabla ya hapo alimanusura nao Newcastle wapate bao kupitia shuti la nje ya kumi na nane la Sean Longstaff lililopiga besela.

Chelsea, ambao walikuwa nafasi ya tano wamepanda mpaka nafasi ya kwanza kwa tofauti ya magoli na Leicester City ambao watakuwa ugenini siku ya Jumapili dhidi ya Majogoo wa Jiji la Merseyside Liverpool.

Author: Bruce Amani