Cherono ahifadhi taji la Berlin Marathon

Mkenya Gladys Cherono alihifadhi taji lake la Berlin Marathon kwa upande wa wanawake baada ya kuweka muda bora wa 2:18:11. Alimaliza mbele ya Muethiopia Aga Ruti aliyetimka katika muda wa 2:18:35 na Muethiopia mwenzake Tirunesh Dibaba aliyemaliza wa tatu katika muda wa 2:18:56.

Ulikuwa ni ushindi wa Cherono wa tatu mfululizo katika Berlin Marathon katika siku ambayo itabakia katika kumbukumbu za wakenya katika mji mkuu wa Ujerumani. Alishinda mbio hizo mwaka wa 2017 kwa kutumia muda wa 2:20:23

Akizungumza baada ya ushindi wake, Cherono alisema lengo lake lilikuwa ni kuvunja rekodi ya muda bora wa mbio hizo na kukimbia chini ya 2:19:00. “Nna furaha sana kuweza kuweka rekodi mpya katika mbio hizi za Berlin. Hali ya hewa ilikuwa nzuri na ikanifanya kukimbia kwa kasi”. Alisema Cherono. Sasa malengo yake ni kurudi Berlin mwaka ujao na kujaribu kuivunja rekodi hiyo tena.

Muda aliouweka Cherono ndio wa nne wa kasi zaidi katika historia ya marathon kwa wanawake baada ya Muingereza Paula Radcliffe (2:15:25), Mkenya Mary Keitany (2:17:01) na Muethiopia Tirunesh Dibaba (2:17:56)

Author: Bruce Amani

Share With Your Friends