Madai ya Gianni Infantino kuwa siku za ufisadi katik FIFA zimezikwa katika kaburi la sahau yamepata pigo kufuatia uchunguzi wa jinai unaofanywa dhidi ya rais huyo wa shirikisho la kandanda ulimwenguni. Patashika Viwanjani leo inakufahamisha uchunguzi huo una maana gani. Mimi ni Bruce Amani.
Uchunguzi wa jinai wa waendesha mashitaka wa Uswisi dhidi ya Rais wa FIFA Gianni Infantino ni mfano wa karibuni wa shirkisho hilo la kandanda ulimwenguni kugubikwa na madai ya ufisadi.
Mashitaka ya ufisadi uliokita mizizi katika taasisi hiyo yaliwang’oa maafisa kadhaa wa ngazi ya juu mwaka wa 2015, akiwemo aliyekuwa rais wa muda mrefu Sepp Blatter. Mtu aliyetwikwa mzigo wa kurejesha hadhi ya FIFA wakati uchunguzi ukiendelea nchini Marekani na Uswisi alikuwa Infantino.
Hata hivyo, mtu aliyechaguliwa katika Mkutano wa Baraza kuu la FIFA Juni 2016 na kuchaguliwa tena Juni 2019, sasa anajikuta katikati ya uchunguzi wa jinai unaoongozwa na mwendesha mashitaka mkuu wa Uswisi Stefan Keller.
Mbona Rais wa FIFA Gianni Infantino anachunguzwa?
Keller alitangaza Alhamisi kuwa kulikuwa na “ishara za muenendo wa kihalifu” katika mikutano ambayo haikutangazwa kati ya Infantino na Mwanasheria Mkuu wa Uswisi Michael Lauber ambaye ataondoka katika wadhifa huo mwezi ujao.
Mikutano hiyo mitatu, inayodaiwa kufanyika kati ya 2015 na 2016, ni muhimu kwa sababu Lauber, kwa wakati huo, akisimamia uchunguzi wa kashfa ya ufisadi ya 2015 ambayo ilipelekea kufunguliwa mashitaka ya jinai dhidi ya maafisa kadhaa wa FIFA.
Infantino anasisitiza kuwa mikutano hiyo ilikuwa jaribio halali la kusaidia katika uchunguzi.
Infantino anatuhumiwa kwa kosa gani?
Infantino anachunguzwa kwa misingi ya “matumizi mabaya ya ofisi ya umma, uvunjaji wa kanuni ya usiri, kuwasiaidia wahalifu na uchochezi wa kuvunja sheria.”
Hii sio mara ya kwanza kwa Infantino kukabiliana na tuhuma za aina hii, ambazo kwanza zilizuka mwaka wa 2017 kutokana na barua pepe zilizovujishwa na nyaraka za Football Leaks ambazo ziliorodhesha mikutano mitatu katika kipindi cha miezi 15. Infantino na Lauder wote wanadai hawawezi kukumbuka kilichotokea wakati wa matukio hayo. Uchunguzi wa sasa ni kutokana na malalamiko ya jinai kutoka kwa watu wasiojulikana ambayo yalipelekea Keller kuteuliwa kuwa mwendesha mashitaka mkuu wa serikali mwezi Julai. Infantino anayaelezea malalamiko hayo kuwa ya “kipuuzi.”
Hilo lina umuhimu gani?
FIFA ni shirikisho la soka Ulimwenguni, linahusika na kiasi kikubwa cha fedha pamoja na tamasha maarufu sana linalotazamwa na wengi duniani, Kombe la Dunia.
Hadhi yake ilichafuliwa mwaka wa 2015 wakati kukiwa na madai ya utakatishaji fedha na maswali kuhusiana na uhalali wa utoaji zabuni za kuandaa Kombe la Dunia 2018 na 2022 nchini Urusi na Qatar.
Hata ingawa walimleta Infantino kuusafisha uchafu huo, bado wanapambana kujiondoa katika wingu la ufisadi ambao liligubika mwishoni mwa utawala wa Blatter.
Kwa nini Gianni Infantino bado ni Rais wa FIFA?
Kwa sababu FIFA hawaendeshwi kama kampuni ya kawaida ya shirikisho la usimamizi. Ilichukua miaka mingi ya madai mazito kuhusiana na matukio ya kihalifu na hongo, kabla ya Sepp Blatter kusitishwa kuwa rais wa shirikisho hilo.
Blatter alidai kuwa angevuliwa tu wadhifa wake kupitia kura yakiwemo mataifa yote wanachama. Lakini ilibidi kamati ya maadili ya FIFA iingilie kati na kumpiga marufuku Blatter kushiriki katika shughuli zote zinazohusiana na kandanda kwa miaka minane.
FIFA imetoa taarifa ya kumuunga mkono Infantino kufuatia uchunguzi huo na Infantino amesema atashirikiana kikamilifu na mchakato huo wa kisheria.
Nini kinafuata sasa?
Wakati imeelezwa kuwa mwendo wa uchunguzi wa kumfungulia mashitaka Infantino umekuwa wa kasi zaidi ukilinganisha na mtangulizi wake Blatter, hakuna uwezekano kuwa kesi hiyo itafikishwa katika mahakama ya jinai au kutolewa kwa hukumu.
FIFA wamesisitiza bado wako tayari “kushirikiana kikamilifu” na maafisa wa Uswisi kuhusu suala hilo, wakidai kuwa ushirikiano wao katika siku za nyuma ulisaidia katika “kuhukumu kesi 40 za uhalifu.” Na watatumai kuwa kesi nambari 41 haitamhusisha rais wao wa sasa.
Chanzo: DW Sports