City, Chelsea na Liverpool zafungana kileleni

62

Manchester City, Chelsea na Liverpool zimefungana kileleni mwa msimamo wa ligi ya England, PL, wakati timu zote zikifikisha pointi 20, baada ya Riyaz Mahrez kushindwa kuutumia vyema mkwaju wa penati na kulazimisha Man City na Liverpool kutoka sare ya bila kufungana, katika uwanja wa Anfield.

Chelsea, iliyokuwa ugenini na ambayo haijashindwa katika mechi nane iliwabamiza Southampton mabao 3-0, wakati Arsenal inayoshika nafasi ya nne ikiwa na pointi 18, nayo ikicheza ugenini iliwanyeshea mvua ya magoli Fulham baada ya kuwachabanga mabao 5-1, na kujiwekea rekodi ya ushindi wa sita mfululizo kwenye ligi ya Premier.

Kwingineko, Tottenham imeendelea kutetea kampeni yake ya ubingwa baada ya ushindi wa 1-0 dhidi ya Cardiff inayoburuta mkia, huku Manchester United inayoyumba nayo ikirejea dimbani kwa kishindo kufuatia ushindi wa kutokea nyuma wa mabao 2-0 hadi 3-2 dhidi ya Newcastle, katika uwanja wa nyumbani wa Old Trafford.

Walikuwa ni Juan Mata, Alexis Sanchez na Anthony Martial waliookoa kibarua cha kocha Jose Mourinho, anayekabiliwa na shinikizo kutokana na mwanzo mbovu wa msimu wa klabu hiyo.

Author: Bruce Amani