Clatous Chama ni mali ya Simba na haendi kokote: Mo Dewji

732

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Simba, Mohamed Dewji amefuta tetesi ambazo zilikuwa zikimhusisha kiungo mshambuliaji wa timu hiyo Clatous Chota Chama kutua kunako klabu ya Yanga katika dirisha dogo la usajili la mwezi Januari. Mo Dewji amesema mkataba wao na Chama unaisha mwaka 2022, hivyo taarifa za kuwa anakwenda Yanga zimekuwa zikiwashangaza.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo Jumapili, Dewji amesema mchezaji huyo ni mali ya Simba na hakuna sababu ya kuwa na hofu.

“Taarifa sijui anakwenda Yanga ni mambo ambayo si sahihi, hakuna sababu ya kuwa na hofu na ninawatoa hofu mashabiki wa Simba kuwa tuko makini sana.

“Sehemu mbalimbali zimekuwa nikikutana na mashabiki wa Simba ambao wananiambia Mo fanya Chama asiondoke Simba. Chama ni mchezaji wa Simba.

“Suala kwamba anakwenda Yanga sijui linatoka wapi lakini haina shida, sasa nimewaambia na ninafikiri leo tunafunga mjadala,” alisema Mo Dewji.

Siku za karibuni kumekuwa na ripoti mbalimbali zinazomhusisha Chama raia wa Zambia kuwa anamaliza mkataba wake mwezi Juni mwakani hivyo anaweza akatua sehemu yoyote kama mchezaji huru lakini kutokana na maneno ya Mo Dewji huenda tukaona Mwamba huyo wa Lusaka akiendelea kukitumikia kikosi cha Wekundu wa Msimbazi Simba.

Author: Asifiwe Mbembela