Corona yasababisha sintofahamu Serie A, Juventus kupewa pointi za mezani baada ya Napoli kushindwa kufika uwanjani wakiwa wamejitenga karantini

Katika hali isiyokuwa ya kawaida, mchezo wa Serie A kati ya Juventus na Napoli uliopagwa kuchezwa leo Jumapili katika dimba la Turin haujachezwa lakini timu ya Juve huenda wakapewa alama tatu za mezani.

Baada ya vipimo kuonyesha watu wawili ndani ya klabu ya Napoli kuwa na maambukizi wiki hii, waliamuriwa kutosafiri na kujitenga ikiwa ni sehemu ya kulinda afya za wananchi na kutii mamlaka ya afya eneo lao, walisema Napoli.

Shirikisho la Soka nchini Italia ilikataa maombi ya Napoli ya kuahirisha mchezo huo wakitaka uchezwe kama kawaida licha ya ripoti kudai maambukizi hayo.

Klabu ya Juventus walifika uwanjani lisaa limoja kabla kwa maana ya 21:45 usiku lakini walikosa mpinzani wa kucheza nae.

Kwa mjibu wa sheria za Serie A, Juventus watapewa alama tatu na ushindi wa mezani wa goli 3-0 baada ya mchezo ambao uliotakiwa kuchezwa leo timu ya Napoli kutofika uwanjani.

Viongozi wa Ligi wamesema Mamlaka ya Afya Naples (ASL) walishindwa kutoa mwongozo wa afya ambao ulikubaliiwa baina ya Wizara ya afya na michezo ya taifa hilo na Mamlaka za soka.

Makubaliano baina ya pande hizo nne yalikuwa yanasema, kama itabainika kuwa mchezaji/wachezaji wameathirika na virusi wataendelea kufanya mazoezi na watacheza mechi. Taarifa hiyo iliongeza kuwa mechi nyingi msimu huu zimechezwa baada ya kubainika kuwa mchezaji/wachezaji wamepimwa na kukutwa na maambukizi.

Jumapili iliyopita Napoli ilicheza dhidi ya Genoa wakati ambao wachezaji 17 wa timu hiyo walikuwa wamepimwa na kukutwa na maambukizi ya Covid-19.

Ingawa mchezo wa Genoa na Torino siku ya Jumamosi ulihairishwa.

Serie A katika kanuni zake zinasema mechi itaendelea kama kawaida endapo timu husika itakuwa na wachezaji angalau 13, tofauti yake endapo timu moja ndani ya wiki moja itathibitika kuwa mchezaji/wachezaji wake 10 wamekutwa na maambukizi ya virusi mechi yao itatuhusiwa kuhairishwa bila kukatwa pointi.

Juventus hata kikosi chao hakijatengamaa baada ya viongozi wawili kukutwa na maambukizi ya Covid-19 siku za karibuni.

Siku ya Jumamosi Octoba 3, zilitoka ripoti zikidai kuwa Napoli haitasafiri kwenda Turin kutokana na janga la virusi vya Corona, lakini kupitia mtandao wao wa Twitter Juventus waliandika wataipeleka timu uwanjani kutimiza kanuni za Seria A.

Siku ya mechi Jumapili kupitia ukurasa rasmi wa Twitter Juve waliendelea kutoa taarifa mbalimbali za maandalizi ya mchezo huo kama kuwaonyesha wachezaji wakiingia uwanjani sambamba na kikosi cha mchezo husika.

Author: Asifiwe Mbembela