De Gea aivunja mioyo ya Spurs na kuwapa United pointi tatu

15

Jina lake liliimbwa na mashabiki na kupongezwa sio tu na waumini wa hekalu la Old Trafford bali pia mashabiki wa kandanda kote ulimwenguni. Kipa wa Manchester United David De Gea alionyesha umahiri wake uwanjani Wembley wakati kaimu kocha Ole Gunnar Solskjaer akipata ushindi wake wa sita katika mechi sita na kuvuruga malengo ya Tottenham kutwaa ubingwa wa Ligi ya Premier

Chipukizi Marcus Rashford alifunga bao safi kupitia counter attack baada ya kuandaliwa pasi safi na Paul Pogba muda mfupi kabla ya kipindi cha kwanza kukamilika, lakini United watamshukuru sana kipa wao De Gea aliyedhihirisha usogora wake langoni na kuyazima mashambulizi chungu nzima ya Spurs, na hasa katika kipindi cha pili.

Mhispania huyo alifanya maajabu kwa kuokoa jumla ya makombora 11 mfululizo, yakiwemo mengi aliyookoa kwa mguu wake, wakati Spurs walijaribu bila kufua dafu kuepuka kichapo ambacho kinafanya sasa kazi yao ya kufukuzana na Liverpool na Manchester City kuwa ngumu zaidi.

De Gea aliivunja mioyo ya Spurs na mashabiki wake kwa kuwazima Harry Kane mara kadhaa pamoja na Dele Alli na Toby Alderweireld.

Matokeo hayo yameiacha Spurs pointi tisa nyuma ya vinara Liverpool na United pointi sawa na nambari tano Arsenal wakati wakiyafufua matumaini yao ya kutinga nafasi nne bora.

Author: Bruce Amani