De gea asema kipigo ni aibu, amtetea Solskjaer

Kipa wa Manchester United David de Gea amesema kipigo ambacho timu yake imekipata cha kupoteza goli 4-1 dhidi ya Watford ni aibu isiyovumilika.

United inapoteza mechi nyingine ambapo sasa imeangukia kwenye nafasi ya saba msimamo wa Ligi ikiwa imeshinda mechi moja pekee katika mechi saba ambapo sasa presha kwa kocha Ole Gunnar Solskjaer inaongezeka naradufu.

Machungu zaidi kwa Man United ni kuwa hata nahodha wao Harry Maguire akaonyeshwa kadi nyekundu wakati huo huo beki Raphael Varane ni majeruhi.

“Kwa namna ambavyo tumefungwa ni aibu, inasikitisha”, alisema David de Gea baada ya kumalizika kwa mchezo wa Watford ambapo aliokoa michomo miwili ya penati.

“Kipindi cha kwanza tulikuwa hovyo, haikubaliki kwa klabu kama hii na wachezaji tuliopo hapa. Kwa kweli ni vigumu hata neno la kusema”.

“Ni rahisi kusema na kulituhuma bechi la ufundi akiwemo kocha lakini sisi ndiyo tunakuwa uwanjani tunatakiwa kupambana, kufunga magoli na kuhakikisha tunapata matokeo. Binafsi nasema ni vigumu kujua kwa nini tuko kwenye kiwango kama hiki”, alisema David de Gea ambaye ni miongoni mwa wachezaji wakongwe klabuni hapo.

Author: Asifiwe Mbembela

Share With Your Friends