Di Maria aongoza maangamizi ya PSG dhidi ya Marseille

48

Angeweza kufunga hat trick kama angeamua kupiga penalti ambayo ilipotezwa katika dakika ya mwisho ya mchezo. Angel Di Maria alionyesha mchezo safi sana kwa kufunga mabao mawili na kupeana pasi ya bao la tatu wakati mabingwa watarajiwa wa ligi ya Ufaransa Paris Saint-Germain ikiizaba Olympique Marseille iliyokuwa pungufu mchezaji mmoja mabao 3-1

Mshambuliaji huyo Muargentina huyo aliwatatiza sana mabeki wa Marseille mechi nzima, alipoongeza bao la pili baada ya Kylian Mbappe kufungua ukurasa wa magoli. PSG sasa wana pointi 77 katika mechi 28.

Marseille, mahasimu wakali wa PSG ambao walisawazisha kupitia Valere Germain sekunde chache baada ya kipindi cha pili kuanza, wako nafasi ya nne na pointi 47 kutokana na mechi 29.

Kipa wa OM Steve Mandanda alipewa kadi nyekundu baada ya dakika 62 kwa kuunawa mpira katika eneo hatari.

Mapema Jumapili, nambari tatu kwenye ligi Olympique Lyonnais ilipata ushindi wa 3 – 2 dhidi ya Montpellier na wakawakaribia Lille na pengo la pointi nne. Lille walilazwa 1 – 0 na Monaco siku ya Ijumaa na sasa wako nafasi ya pili nyuma ya PSG na tofauti ya pointi 20 wakiwa wamecheza mechi moja zaidi.

Author: Bruce Amani