Djuma, Moloko warejea Yanga kuivaa KMC

Msemaji wa klabu ya Yanga Hassan Bumbuli ametolea ufafanuzi wa kutoonekana kwa baadhi ya wachezaji wa kimataifa katika kambi ya timu hiyo hasa kwenye mchezo wa kirafiki na JKU ya Zanzibar ambapo amesema walikuwa wameomba ruhusa ya kurudi nyumbani kwa ajili ya kushungulikia masuala ya hati ya kusafiria.

Miongoni mwa wachezaji ambao hawakuonekana kwenye mechi hali kadhalika katika mazoezi ya timu ni winga Jesus Moloko na beki wa kulia Djuma Shaban ambao wote hati zao za kusafiria zilikuwa zinaelekea kutamatika hivyo kulazimika kurudi Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kupata suluhu.

Hata hivyo wachezaji hao tayari wamerejea nchini na kuanza mazoezi na wenzao yakiwa ni maandalizi ya mechi dhidi ya Kinondoni Municipal Council (KMC), mtanange utakaopigwa mkoani Songea.

Taarifa ya Bumbuli inafuatia na kile kilichoelezwa kuwa wachezaji hao akiwemo mlinda mlango namba moja wameondoka kambini bila kufuata utaratibu jambo lililokuwa limeanza kuanzisha minong’ono miongoni mwa wadau wa michezo nchini.

Author: Asifiwe Mbembela

Share With Your Friends