Dortmund yaangazia patashika ya siku ya mwisho ya msimu

Afisa Mkuu Mtendaji wa klabu ya Borussia Dortmund Hans-Joachim Watzke amesema kuwa shinikizo sasa liko kwa vinara wa ligi Bayern Munich baada ya timu yake kurejea tena katika kinyang’anyiro cha ubingwa wa ligi ya Ujerumani – Bundesliga hapo jana.

Bayern walikosa nafasi ya kunyakua taji lao la saba mfululizo baada ya kutoka sare tasa na RB Leipzig, wakati Dortmund ikiifunga Fortuna Düsseldorf 3 – 2 na kujiweka tena katika mbio za ubingwa hadi mechi za mwisho wikiendi ijayo.

Watzke amesema sasa wao wanastahili kushinda tu, na kisha wasubiri matokeo ya Bayern.

Katika mechi iliyokuwa na shinikizo kubwa, Bayern walipata bao lakini likafutwa na mfumo wa VAR baada ya mshambuliaji Robert Lewandoswki kuonekana kuwa ametoea.

Katika dimba la Signal Iduna Park, Christian Pulisic ambaye ataondoka mwishoni mwa msimu huu, alicheza mechi yake ya mwisho mbele ya mashabiki wa nyumbani na akafunga bao la kwanza. Mabao mengine ya BVB yaliwekwa wavni na Thomas Delaney na Mario Gotze.

Bayern watacheza dhidi ya Eintracht Frankfurt Jumamosi ijayo wakiwa na faida ya kuwa katika uwanja wa nyumbani wakati Dortmund watakuwa ugenini dhidi ya Borussia Moenchengladbach

Author: Bruce Amani

Share With Your Friends