Dortmund yaendeleza ubabe kwa kuibamiza Atletico

98

Michuano ya Jumatano ya Champions League ilitifua vumbi huku kukiwa na mambo kadhaa ya kuangaziwa katika mechi nane zilizochezwa za hatua ya makundi.

Borussia Dortmund iliipa kipigo Atletico Madrid, ambayo ni makamu bingwa wa Champions League mara mbili katika misimu mitano. Axel Witsel aliwaweka kifua mbele katika kipindi cha kwanza kabla ya Raphael Guerreiro kuingia kama nguvu mpya na kuongeza mawili katika kipindi cha pili. Chipukizi wa Uingereza Jadon Sancho alikamilisha mvua ya magoli alipoongeza la Dortmund la nne zikiwa zimesalia dakika saba mechi kukamilika.

Mchuano kati ya vigogo Barcelona na Inter Milan ulikosa huduma za Lionel Messi lakini haukukosa uhondo hata ingawa timu hizo zilicheza kukiwa na goli moja tu kwa dakika 82 za kwanza. Rafihna aliipa Barca uongozi katika dakika ya 32. Jordi Alba aliwahakikishia Barca pointi tatu katika dakika ya 83 na kuwapa shindi wa 2-0 ambao unawaweka kileleni mwa Kundi B.

Mohamed Salah alifunga mabao mawili katika usindi wa Liverpool wa 4-0 nyumbani dhidi ya Red Star Belgrade. Mabao mengine ya Reds yalifungwa na Roberto Firmino na Sadio Mane na kuiweka Liverpool kileleni mwa Kundi C

Nchini Ufaransa, bao la kusawazisha la dakika ya mwisho lake Angel Di Maria liliiokoa Paris Saint-Germain kutopata kipigo dhidi ya Napoli, ambapo mchuano ulikamilika kwa sare ya 2-2.

Mchuano wa kwanza wa Champions League wake Thierry Henry kama kocha wa Monaco haukwenda kama alivyopanga. Walitekwa kwa sare ya 1-1 na Club Brugge ya Ubelgiji.

Mjini Istanbul, Galatasaray na Schalke zilitoka sare tasa baada ya kila mmoja kukosa kuona lango la mwenzake.

Porto ilipata ushindi wa 3-1 ugenini dhidi ya Lokomotiv mjini Moscow huku nchini Uholanzi, Totenham Hotspur ilishindwa kupata pointi zote tatu baada ya kulazimishwa kwa sare ya 2-2 na PSV.

Author: Bruce Amani