Eto’o, Drogba waondoa tofauti zao, sasa waungana katika hili

Didier Drogba ambaye alivuma na Chelsea akiipa ubingwa wa Uefa Champions League mbele ya Bayern Munich iliyokuwa bora na Samwel Eto’o, staa wa zamani wa Barcelona na Cameroon kwa pamoja wameshindwa kuafikiana na mpango wa madaktari wa Ufaransa wanaopambana kupata kinga ya virusi vya corona vinayosababisha homa kali ya mapafu.

Eto’o na Drogba wamepinga vikali kuhusiana na maprofesa wawili nchini Ufaransa ambao wamependekeza kuwa majaribio ya kinga ya corona (BCG vaccine) yaje kufanyiwa kwa watu wa Afrika, kitu ambacho kimetafsiriwa na wao kama ubaguzi wa rangi na kuwakosea heshima wa Afrika ambao ni binadamu kama walivyo wazungu.

Camille Locht ambaye ni profesa, kupitia moja kati ya vituo vya TV nchini Ufaransa alisema “Kiukweli tunafikiria njia tofauti kiupana kufanya mafunzo Afrika kwa ajili ya kufanya majaribio ya BCG lakini haijatuzuia pia kufikiria kufanya majaribio haya ndani ya Ulaya na Afrika”.

Nahodha wa zamani wa Ivory Coast Didier Drogba aliandika kupitia twitter account yake “Haikubaliki kabisa kuendelea kukubaliana na hili kwa nguvu nakemea hili ubaguzi wa rangi na kuendelea kudharauliwa, tusaidieni kuokoa maisha Afrika na kuzuia kuenea kwa virusi ambavyo vitaenea dunia nzima, badala ya kutuchukulia kama nguruwe”

Staa wa zamani wa Inter Milan na timu ya taifa ya Cameroon Samuel Eto’o alionesha hasira zake baada ya kusikia hayo kupitia ukurasa wake wa instagrama kwa kuandika “Afrika sio yenu kiasi cha kufikiria mnaweza kuichezea vyovyote vile”.

Hizo ni kauli za wachezaji wenye hadhi kubwa Afrika huenda hata mpango wa wataalamu hao juu ya kuja kufanya majaribio huku Afrika ukaota mbawa.

Author: Bruce Amani