Dube awapiga chenga Metacha, Mwijage VPL

Staa wa timu ya Azam Fc ya Jijini Dar es Salaam, Prince Dube amechaguliwa kuwa Mchezaji Bora wa mwezi Mei wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania (VPL), msimu wa 2020/21.

Dube alitwaa tuzo hiyo baada ya kuwashinda wenzake walioingia nao fainali kwa mwezi Mei katika uchambuzi uliofanywa mwishoni mwa wiki iliyopita na Kamati ya Tuzo za VPL, kutokana na mapendekezo ya makocha waliopo viwanja mbalimbali nchini.

Mshambuliaji huyo alikuwa na mchango mkubwa kwa timu yake mwezi Mei na kuonesha kiwango cha kuvutia akifunga mabao mawili na kuhusika katika bao moja, ambapo Azam ilicheza michezo miwili na kushinda yote.

Wengine walioingia fainali ni mchezaji wa Kagera Sugar, Erick Mwijage pamoja na kipa wa Yanga, Metacha Mnata ambao walikuwa na kiwango kizuri kwa mwezi huo.

Hiyo ni mara ya pili kwa Dube kutwaa tuzo hiyo, ambapo mara ya kwanza ilikuwa Septemba mwaka jana, pia Aprili aliingia fainali na kushindwa na kiungo Clatous Chama wa Simba.

Mwingine aliyeingia fainali Aprili alikuwa Raphael Daud wa Ihefu SC.

Author: Asifiwe Mbembela

Sharing is caring!

0Shares