Eliud Kipchoge ashinda tuzo ya mwanariadha bora wa mwaka

Bingwa wa dunia wa mbio za Marathon Mkenya Eliud Kipchoge na Mcolombia, Caterine Ibarguen anayeshiriki mashindano ya kuruka – high jump, long jump na triple jump ndio wanariadha bora wa mwaka 2018.

Kipchoge ameshinda tuzo hii baada ya mwezi Septemba kuvunja rekodi ya mbio za Marathon Berlin Ujerumani kwa muda wa saa mbili dakika moja na sekunde 39.

Mwanariadha huyo wa Kenya mwenye umri wa miaka 34, anatajwa kuwa mwanariadha bora wa mbio hizi ndefu katika miaka ya hivi karibuni.

Kati ya mashindano 11 ya Marathon aliyoshiriki, ameshinda 10 na kushinda mara tatu jijini London na Berlin bila kusahau wakati wa michezo ya Olimpiki mwaka 2016 nchini Brazil.

Author: Bruce Amani