England yaiduwaza Poland jioni kwa bao la Harry Maguire

368

Timu ya Taifa ya England ilihitaji bao la dakika za lala salama la mlinzi wa kati wa Manchester United Harry Maguire kuvuna alama tatu katika mchezo wa tatu wa kuwania nafasi ya kufuzu Kombe la Dunia Qatar 2022 dhidi ya Poland mtanange uliopigwa dimba la Wembley Jumatano.

Poland ambao walimkosa nyota wao Robert Lewandowski kutokana na majeruhi walionekana kuwa mtihani mkubwa kwa England kuliko ilivyokuwa kwenye mechi mbili za nyuma dhidi ya San Marino na Albania na walionekana kuenda kupata alama moja kwa sare lakini shuti la Maguire limefuta uwezekano huo.

England walianza kutangulia kupata goli kupitia kwa mshambuliaji Harry Kane lakini bao hilo lilisawazishwa na Jakub Moder kufuatia makosa ya mlinzi wa kati wa Manchester City John Stones.

England wamefanikiwa kuvuna alama tatu kwenye kila mechi tatu zilizopita za kufuzu Kombe la Dunia. Poland bado wana nafasi nzuri kufuzu kuingia Kombe la Dunia.

Author: Asifiwe Mbembela