Euro 2020 yaahirishwa rasmi mpaka 2021

Mashindano ya Euro 2020 yameahirishwa kwa mwaka mmoja hadi 2021 kutokana na hofu ya Virusi vya Corona ambavyo vimeenea maeneo mengi duniani.

Kauli hiyo ya kuahairisha michuano hiyo imeitoa Shirikisho la Mpira wa Miguu Uingereza FA leo Jumanne baada ya kikao cha wazi na wadau mbalimbali kujadili hatima ya mashindano hayo.

Katika kikao kilichohusisha Uefa, Uongozi wa Soka Ulaya sambamba na wadau wa soka wamefanya kikao cha video kilichokuwa na kusudi la kujadili mstakabali wa Euro 2020 ambapo kwa pamoja wameafikiana kuhairisha mashindano hayo.

FA imesema kuwa mashindano yajayo yanafanyika kuanzia Juni 11 mpaka Julai 11 mwaka 2021.

Aidha, mashindano ya mwaka huu yalipangwa kuanza kuchezwa Juni 12 mpaka Julai 12 katika viwanja 12 tofauti barani Ulaya.

Baadhi ya wachambuzi wa masuala ya soka wamekuwa wakizungumza kuwa kuhairishwa kwa michuano hiyo ni kutoa muda zaidi wa Ligi barani Ulaya kumalizika.

Michuano ya Ligi ya Mataifa Ulaya na michuano ya vijana chini ya umri wa miaka 21 imepangwa kufanyika msimu ujao.

Ugonjwa wa Corona, unaambukizwa kwa hewa ambapo dalili zake ni kama kukohoa, na kuhema kwa shida, kukosa hamu kula, mpaka sasa umeenea kwa kiwango kikubwa ambapo zaidi ya watu 116,000 wameathirika na Virusi hivyo duniani.

Wanasayansi wamethibitisha kuwa ugonjwa huo unahitaji siku tano pekeee kuonyesha dalili zake.

Author: Bruce Amani

Facebook Comments