Everton wavunja rekodi ya miaka 22 kuwafunga 2-0 Liverpool katika ngome yao ya Anfield

Everton imeibuka na ushindi wa goli 2-0 dhidi ya Liverpool katika dimba la Anfield kwa mara ya kwanza katika miaka 22 ambayo vilabu hivyo vimekutana kwenye mechi mbalimbali za kimashindano.

Mara ya mwisho Everton kuondoka na alama tatu au ushindi katika dimba hilo ilikuwa mwaka 1999.

Mbali na hivyo, unakuwa ushindi wa kwanza kwa Everton mbele ya Liverpool tangia mwaka 2010 mbali na Anfield, inakuwa mara ya kwanza kwa kikosi cha Liverpool kupoteza mechi nne mfululizo nyumbani (Anfield) tangia mwaka 1923.

Everton walijipatia magoli kupitia kwa mshambuliaji wa kimataifa wa Brazil Richarlison dakika za mapema kabisa ungwe ya kwanza akimalizia pasi ya James Rodriguez kabla ya kufunga goli la pili la penati iliyowekwa kimiani na kiungo mshambuliaji na nahodha wa kikosi hicho Gylfi Sigurdsson baada ya Dominic Calvert-Lewin kufanyiwa madhambi na Trent Alexander-Arnold.

Mpaka dakika tisini zinakamilika, ilikuwa kicheko kwa Meneja Carlo Ancelotti wakati mwendelezo mbaya kwa kocha Jurgen Klopp ukiendelea huku sababu kubwa ikiwa ni majeruhi kwa wachezaji wake, swali Wanaliverpool watasubiri ni mpaka lini kurejea kwa nyota wao?.

Author: Bruce Amani

Sharing is caring!

0Shares