Fainali ya Champions League kati ya Esperance na Wydad kurudiwa

Shirikisho la Kabumbu barani Afrika, CAF, limeamuru duru ya pili ya fainali ya kombe la vilabu bingwa barani humo, kati ya Esperance ya Tunisia na Wydad Casablanca ya Morocco, irudiwe kwenye uwanja huru, baada ya kumalizika kwa mashindano ya kombe la mataifa barani Afrika yanayofanyika mwezi huu nchini Misri. Klabu ya Esperance ya Tunisia, ilikabidhiwa kombe hilo hapo awali, baada ya Wydad Casablaca kuondoka uwanjani katikati ya pambano kwa sababu ya kukosekana kwa teknolojia ya uchunguzi – VAR, kuamua juu ya goli la kusawazisha lililokataliwa.

Mabingwa Esperance walikuwa wanaongoza kwa bao 1-0 katika duru ya pili na 2-0 kwa ujumla wakati mechi hiyo iliposimamishwa, na baada ya kucheleweshwa kwa dakika 90, mwamuzi aliitangazia ushindi wa Esperance ambao ndiyo waliokuwa wenyeji wa mechi hiyo ya marudio. Afisa wa Esperance amesema watapinga uamuzi huo kwenye mahakama ya kutatua mizozo ya kimichezo.

Author: Bruce Amani

Share With Your Friends