Farah kushiriki katika 2019 London Marathon

Mwanariadha anayeshikilia rekodi ya Ulaya Mo Farah atashiriki katika mbio za mwaka ujao za London Marathon kwa mara ya tatu. Waandalizi wa mashindano hayo wamethibitisha hayo leo Jumanne.

Bingwa huyo wa Olimpiki, Dunia na Ulaya katika mbio za Mita 10,000 na 5,000 alistaafu kutoka mashindano ya ndani ya uwanja baada ya msimu wa 2017 ili kushiriki kikamilifu katika mbio za marathon baada ya kujitosa katika mbio hizo kwa mara ya kwanza mjini London mwaka wa 2014.

Katika mbio za mwaka huu, alimaliza katika nafasi ya tatu kwa kutumia muda wa saa mbili, dakika sita na sekunde 21, ambapo mshindi alikuwa ni Mkenya Eliud Kipchoge.

Farah alishinda mbio zake za kwanza za marathon kwa kutwaa taji la Chicago Marathon mwezi Septemba mwaka huu kwa kutumia muda wa masaa mawili, dakika tano sekunde 11, ikiwa ndio rekodi ya Ulaya.

Author: Bruce Amani

Share With Your Friends