Fergie akaribishwa kwa heshima Old Trafford

Old Trafford ilimkaribisha mgeni maalum katika mchuano wa Manchester United dhidi ya Wolves, ambaye alipewa heshima kubwa na mashabiki. Mashabiki walinyanyuka kwenye viti vyao na kumpigia makofi kocha wa zamani wa Manchester United Sir Alex Ferguson ambaye alirejea katika uwanja huo kwa mara ya kwanza tangu alipofanyiwa upasuaji wa dharura wa ubongo mwezi Mei.

Ferguson ambaye ana umri wa miaka 76, alisema kabla ya mechi ya leo kuwa imekuwa safari ndefu, lakini kwa sasa anapiga hatua mbele, na kufanya kile madaktari wanamwambia akifanye. Na anajiskia vizuri.

Alipigiwa makofi ilipofika dakika 27 ya mchezo ikiwa ndo idadi ya miaka ambayo Mscotland huyo alikuwa kwenye usukani wa timu hiyo.

Kuwepo kwake hata hivyo hakukuisaidia Manchester kupata ushindi, maana vijana hao walilazimishwa sare ya bao moja kwa moja na Wolves.

Katika matokeo mengine, Tottenham Hotspur ilipata ushindi wa 2-1 dhidi ya Brighton & Hove Albion, Manchester City ikaikandika Cardiff 5-1 huku Liverpool ikirejea kileleni kwa kuilaza Southampton 3-0

Author: Bruce Amani

Facebook Comments