FIFA kuondoa marufuku ya Sierra Leone baada ya kesi

57

Shirikisho la Kandanda Duniani – FIFA linatafakari kuondoa marufuku ya Sierra Leone kutoka kandanda la kimataifa baada ya kesi ya rushwa dhidi ya Rais wa Shirikisho la kandanda la nchi hiyo Isha Johansen kukamilishwa mahakamani.

Maafisa wa FIFA akiwemo Katibu Mkuu Fatma Samoura walikutana Alhamisi na Johansen na serikali ya Sierra Leone ili kujadili suala hilo.

FIFA itasubiri kukamilishwa kwa kesi kabla ya hatua zaidi kuchukuliwa ikiwa ni pamoja na kuondoa marufuku kama itahitajika, imesema taarifa.

Johansen anakabiliwa na kesi pamoja na Katibu Mkuu wa shirikisho la kandanda la Sierra Leone SLFA Christopher Kamara. Wote wanakanusha madai dhidi yao.

Serikali ya Sierra Leone ilituma ujumbe wa ngazi ya juu akiwemo makamu wa rais Mohamed Juldeh Jalloh, mwanasheria mkuu na Waziri wa Sheria Priscilla Schwartz na Lansana Gberie, balozi wa Sierra Leone nchini Uswisi. Waziri Wa michezo hakuhudhuria

FIFA iliizuia kwa muda Sierra Leone wiki mbili zilizopita kwa sababu ya uingiliaji wa mtu wa tatu kwenye uendeshwaji wa maswala ya SLFA ikisema kuwa marufuku hiyo itaondolewa punde Johansen na Kamara watakaporejeshwa.

Michuano miwili ya Sierra Leone ya kufuzu katika fainali za AFCON dhidi ya Ghana, ambayo ilitarajiwa kuchezwa kati ya Oktoba 11-14, ilifutwa na hatapangwa upya kwa sababu ya marufuku hiyo.

Author: Bruce Amani