FIFA yapanga kuzindua mpango wa kuwalinda wanasoka wajawazito

Shirikisho la Soka Duniani FIFA limepanga kuuzindua mpango mpya wa kuwalinda wanamichezo wanaopata ujauzito katikati ya msimu wakikusudia kuwalinda kwa kuwapa likizo ya uzazi ya angalau wiki 14. Kwa mujibu wa Bodi ya Kusimamia Masuala ya Michezo ya FIFA (IFA) inataka kuona Wanawake wengi wanashiriki kwenye shughuli za michezo kama ilivyo kwa wanaume, alisema mwanamama Sarai Bareman ambaye ni Ofisa Mkuu wa soka la wanawake Fifa. Bodi hiyo iliongeza kuwa itapeleka mapendekezo mapya katika mkutano mkuu wa FIFA mwezi Disemba ambao utahusisha washiriki takribani 211 wa mashirikisho yote duniani.

Likizo hiyo ya lazima ya wiki 14 itawahakikishia wachezaji kupokea kiasi cha chini cha thuluthi mbili ya mshahara wanaoupokea kwenye mikataba yao Aidha, bodi hiyo imeongeza kuwa wanawake wengi wamekuwa wakivunjiwa mikataba yao pindi wanapobainika wamepata ujauzito na vilabu vyao jambo ambalo halifai katika maisha yao.

“Wazo hili linakusudia kuwalinda wachezaji wa kike michezoni kabla na baada ya kujifungua mtoto,” alisema Mkuu wa usimamizi wa sheria na kanuni wa Shirikisho Emilio Garcia.

Ambapo kanuni hiyo inaongeza kuwa klabu itawajibika kutoa msaada wa kimatibabu na kimwilii baada ya mwanamke kujifungua. Wakati IFA wakipendekeza hilo, Rais wa Shirikisho FIFA Gianni Infantino alisema muswada huo ni muhimu kipindi kama hiki ambacho soka la wanawake linakua kwa kiasi kikubwa, ambapo amesisitiza kuwa lazima wanamichezo wachukue utamaduni huu mpya.

Kabla ya mapendekezo haya, ilikuwa sio rahisi kwa mwanakandanda wa mwanamke kupata ujauzito katika Ligi zenye ushindani kisha akarejea katika timu hiyo baada ya mtoto kukua ingawa mshindi wa Kombe la Dunia nchini Marekani Alex Morgan, 31, alijifungua na kumlea mtoto kisha akarudi tena klabuni kwake Tottenham Hotspur.

Author: Bruce Amani