Gebrselassie ajiuzulu wadhifa wa chama cha riadha Ethiopia

Mwanariadha mkongwe kutokea nchini Ethiopia Haile Gebrselassie amejiuzulu nafasi ya urais wa chama cha riadha nchini humo akiwa amehudumu miaka miwili kati ya minne ambayo alistahili kukaa madarakani bila kuwepo kwa sababu maalumu ya kujiondoa kwake.

Mwanariadha Gebrselassie mwenye umri wa miaka 45 alionyesha nia ya kujiuzulu wikiendi iliyopita katika hatua za kuachia wadhifa wa urais katika Shirikisho la Riadha nchini Ethiopia, hii ni kupitia barua aliyoandika na chombo cha habari cha Ethiopia Fana kiripoti tukio hilo.

“Kilichotokea juzi (Jumapili) hakikuwa sahihi na ni hatari kwa wanariadha nchini Ethiopia. Nimeona ni heri kutojihusisha na majibizano yasiyokuwa muhimu, na kuamua kukaa pembeni kwa maendeleo ya michezo ya nchi yetu”, Aliandika Haile, bila kuelezea zaidi.

Makamu wa Rais wa Shirikisho hilo ambaye pia ni mshindi wa mbio ndefu aliyejinyakulia medali za dhahabu Derartu Tulu atachukua nafasi yake kabla uchaguzi kufanyika tena kuziba nafasi yake. Alisema.

Gebrselassie mshindi mara mbili wa dhahabu katika mbio za mita 10,000 katika Olimpiki, na bingwa wa mbio kadhaa za marathon, alichaguliwa mwaka 2016 baada ya kuwatuhumu viongozi waliokuwepo kuwa sio wawajibikaji wakati Shirikisho hilo likijiandaa na mashindano ya Olympiki yaliyofanyika Rio nchini Brazil.

Ethiopia ilifanikiwa kushinda medali nane tu na kuwa nafasi ya 44 chini ya wapinzani na majirani zao Kenya.

Author: Bruce Amani

Facebook Comments