Gladbach yaibumburusha Bayern

54

Borussia Monchengladbach kwa mara nyingine tena wamewakosesha usingizi mabingwa wa Ujerumani Bayern Munich baada ya kuwapa kichapo cha 3 -0 katika ngome yao ya nyumbani Allianz Arena. Kichapo hicho kina maana kuwa Bayern sasa hawajapata ushindi katika mechi nne mfululizo za Bundesliga matokeo ambayo yanampa tumbo joto kocha wao Nico Kovac.

Alassane Plea alifunga bao katitika dakika ya 10 baada ya kubadilishana pasi za haraka nje ya kijisanduku na Lars Stindl akatia kimyani la pili baada ya Jonas Hofmann kumpokonya mpira Thiago Alcantara alipojaribu kucheza mpira kwa kuuondosha nyuma.

Bayern waliudhibiti mchezo kabla ya kupatikana tena wakisinzia kupitia shambulizi la kushtukiza wakati Patrick Herrmann alibusu wavu kwa bao la tatu huku zikiwa zimebakia dakika mbili mchezo kumalizika.

Kichapo hicho kimeiweka Bayern katika nafasi ya tano, pointi nne nyuma ya viongozi Borussia Dortmund ambao kwa mara nyingine tena walitoka nyuma na kuwashinda Augsburg 4-3 kwenye dimba la kusisimua uwanjani Signal Iduna Park.

Paco Alcacer, ambaye yuko kwenye mkopo kutoka FC Barcelona, alifunga hat-trick katika mtanange huo.

Alfreð Finnbogason aliwaweka wageni kifua mbele katika kipindi cha kwanza kabla ya Alcacer kusawazisha katika dakika ya 32.

Philipp Max alirejesha uongozi wa Augsburg lakini Dortmund ikarudisha kupitia Alcacer na Mario Gotze.

Michael Gregoritsch alisawazisha na akaonekana kuinusuru timu yake kupata pointi moja katika dakika 87, lakini Alcacer alimalizia shughuli katika dakika ya sit ya muda wa nyongeza kwa kufunga bao lake la tatu la ushindi

Hannover 3-1 Stuttgart

Mabao mawili kutoka kwa Ben Wood na moja kutoka kwa Ihlas Bebou yaliipa Hannover ushindi wa 3-1 dhidi ya Stuttgart. Mario Gomez aliifungia Stuttgart bao la kufutia machozi.

Mainz 0-0 Hertha Berlin

Mainz na Hertha Berlin zilitoka sare tasa katika mchuano mkali wa Jumamosi mchana.

Fortuna Dusseldorf 0-2 Schalke

Mabao kutoka kwa Weston McKennie na Guido Burgstaller yaliipa Schalke  ushindi muhimu ambao ni wao wa pili msimu huu katika Bundesliga wa 2-0 dhidi ya Fortuna Dusseldorf.

Werder Bremen 2-0 Wolfsburg

Davy Klaassen na Johannes Eggestein waliipa Werder Bremen ushindi wa 2-0 dhidi ya Wolfsburg.

Author: Bruce Amani