Godin aipa Atletico ushindi dhidi ya Bilbao

155

Kama haujawai kusikia ama kuona mpango B unavyofanya kazi basi endelea kusoma habari hii jinsi kocha wa Atletico Madrid alivyoifanya ‘Plan B’ yake. Ligi kuu Hispania iliendelea tena Jumamosi hii ambapo kocha Diego Someone alilazimika kumchezesha mlinzi wake Diego Godin katika nafasi ya ushambuliaji hata ingawa mchezaji huyo alikuwa amepata majeraha na ilhali hakuwa amebaki na yeyote wa akiba.

Mpango huu B ulifanya kazi licha ya beki huyo kuwa majeruhi. Pamoja na kwamba alikuwa hawezi kukimbia, Godin alifunga goli la ushindi wa timu yake katika mda wa nyongeza kwenye mchezo uliochezwa uwanja wa Wanda Metropolitano. Kabla ya kukubaliwa goli, mwamuzi alilikataa kwa madai ya kuotea ingawa VAR ikathibitisha kuwa hakuotea na kuwa faida kwa Atletico.

Atletico ilitoka nyuma ya goli mbili kwa bila na hatimaye kushinda 3-2. Mlinzi Godin alijitahidi kuuzuia mpira uliokuwa unaelekea nyavuni lakini ilishindikana na hivyo kufanya klabu ya Athletic kuongoza katika dakika ya 64 ya mchezo huo. Godin alifunga goli kwa kichwa baada ya krosi iliyopigwa na Thomas Partey iliyomkuta Antonio Griezmann aliyeipeleka moja kwa moja kwa Godin ambaye bila ajizi alikwamisha mpira nyavuni.  Ushindi huo unaipeleka Atletico alama moja nyuma ya vinara FC Barcelona ambayo itacheza dhidi ya Real Betis katika uwanja wa Cape Nou siku ya Jumapili.

Endapo Espanyol itashinda dhidi ya Sevilla itakwea mpaka nafasi ya pili au tatu kwa kutegemea matokeo ya michezo mingine. Klabu ya Real Madrid ambayo ipo nafasi ya sita na kupata ushindi wa tatu mfululizo tangu alipoichukua timu kocha wa muda Santiago Solari baada ya Julen Lopetegui kufungashiwa virago, itakuwa ugenini leo Jumapili kuikabili Celta Vigo.

Katika matokeo mengine, Valencia imeendelea kufanya vizuri baada ya kuibuka na ushindi wa1- 0 dhidi ya Getafe baada ya kupewa tuta kwa njia ya VAR. Matokeo hayo yameipaisha Valencia mpaka nafasi ya 14 katika msimamo wa La Liga alama tano juu ya timu zilizo katika mstari mwekundu. Getafe, ipo nafasi ya 10 katika msimamo, haijapoteza mchezo hata mmoja katika mashindano yote kati ya minne.

Real Valladolid, ambayo inamilikiwa na mchezaji wa zamani wa Brazil Ronaldo imeenda mpaka nafasi ya kumi na saba ingawa imetoka sare 0-0 dhidi ya  Elbar ambayo ilikuwa nyumbani. Wakati huo huo, Gerona ipo nafasi ya tisa baada ya sare ya bila kufungana dhidi ya Leganes.

Author: Bruce Amani