Gor Mahia kucheza na Waarabu mechi za makundi CAF

139

Kwa mara nyingine tena, mabingwa wa ligi kuu ya Kenya Gor Mahia watapanga safari ya kuelekea Uarabuni kucheza mechi za makundi ya Kombe la Shirikisho.

Hii ni baada ya kupangwa kundi D pamoja na Zamalek ya Misri, Hussein Dey ya Algeria na Petro Atletico ya Angola kwenye droo iliyofanywa mchana wa leo katika makao makuu ya Shirikisho la Soka barani (CAF) mjini Cairo, Misri.

Gwiji wa timu ya taifa ya Cameroon Patrick Mboma alifanya droo hii pamoja na kaimu katibu wa CAF Anthony Baffoe ambapo Kogalo wataanza mechi hizi dhidi ya mabingwa mara tano wa klabu bingwa barani Zamalek Februari 3 jijini Nairobi.

Baadaye wataelekea Algeria kuchuana na Hussein Dey Februari 13 kisha waelekee Angola kugaragazana na Petro Atletico alikopiga straika wa Harambee Stars Allan Wanga.

Februari 24 watawaalika Hussein Dey jijini Nairobi kisha wasafiri kule Algiers Machi tatu kuchuana nao. Machi kumi watakuwa Misri kumenyana na Zamalek kabla ya kumaliza raundi ya sita nyumbani baina ya Petro Atletico.

“Tutapambana tu japo hatupo vizuri kifedha tunaomba serikali iingilie kati walivyofanya kwenye safari yetu ya Cameroon kwa kutulipia tiketi za ndege,” alisema mwenyekiti Ambrose Rachier baada ya safari ya Limbe walikowaliza wenyeji New Stars de Douala kwa kuwaondoa katika mashindano haya baada ya sare tasa na kufuzu 2-1 kwa ujumla wa magoli.

CAF CONFEDERATION CUP MAKUNDI

KUNDI A: Hassania US Agadir (Morocco), AS Otoho d’Oyo (Congo), RS Berkane (Morocco), Raja Casablanca (Morocco)

KUNDI B: Etoile du Sahel (Tunisia), Enugu Rangers (Nigeria), Salitas (Burkina Faso), CS Sfaxien (Tunisia)

KUNDI C: Zesco United (Zambia), Al Hilal (Sudan), Asante Kotoko (Ghana), Nkana (Zambia),

KUNDI D: Gor Mahia (Kenya), Hussein Dey (Algeria), Petro Atletico (Angola), Zamalek (Egypt)

Author: Bruce Amani