Gor Mahia yaangushwa nyumbani na Berkane katika CAF

48

Gor Mahia imepoteza mchezo wa mkondo wa kwanza wa robo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya RSB Berkane ya Morocco uliochezwa uwanja wa Kimataifa wa Moi jijini Nairobi Jumapili.

Ikiwa katika harakati za kupata goli la kuongoza Gor Mahia ilijikuta ikiangukia pua mapema kupitia goli la kujifunga la kiungo Francis Kahata katika dakika ya 24 kabla ya El Helali kufunga goli la mwisho kunako dakika ya 59.

Mbali na kufungwa mlinda mlango wa Gor Frederick Odhiambo aliibuka shujaa kutokana na kuokoa michumo mingi iliyokuwa inaelekea golini mwake.

Inawezekana Gor Mahia ilingia kwenye mchezo huo ikiwa haina nguvu sawa baada ya mshambuliaji wao Jacques Tuyisenge kukosekana kwenye sehemu ya kikosi hicho huku safu ya ushambuliaji ikiongozwa na mshambuliaji mkongwe wa timu Dennis Oliech.

Matokeo ya kufungwa yanampa kazi kubwa Kocha Hassan Oktay ambaye atalazimika kushinda zaidi ya goli 3-0 katika mchezo wa mkondo wa pili huku akizuia kufungwa hata goli moja.

Aidha, rekodi nzuri ya kufanya vizuri kwenye mashindano ya Kombe la Shirikisho hatimaye imefikia kikomo baada ya kukubali kipigo cha aibu uwanja wa nyumbani huku ikiongoza umiliki wa mpira kwa asilimia 61/39.

Author: Bruce Amani