Gor wabeba Super Cup baada ya kuwabwaga Bandari

Mabingwa wa KPL, Gor Mahia wamenyakua taji lao la kwanza la msimu huu baada ya kuifunga Bandari FC mabingwa wa FA msimu uliopita kwa goli 1 – 0 katika mchezo wa Super Cup (Ngao ya Jamii) uliofanyika dimba la Machakos Jumapili.
Kombe hilo linakuja chini ya kocha mpya kwa Gor. Huyu ni Steven Polack, ambaye ameshinda taji lake la kwanza tangu achukue kijiti cha kuinoa Gor Mahia ambapo ameiongoza kuifunga Bandari FC
Gor walilazimika kucheza pungufu kuanzia dakika ya 13 ya mchezo, Tobias Otieno alipoonyeshwa kadi nyekundu baada ya kadi mbili za njano licha ya kucheza pungufu walifanikiwa kubeba taji hilo kwa mara ya sita.
“Naweza kusema ni bahati kwa kupata matokeo haya kwani nimeanza kuifundisha timu hii sio zaidi ya wiki mbili. Hatujacheza vizuri lakini cha msingi tumepata kombe,” Alisema kocha mpya wa Gor Mahia Polack.
Upande wa Bandari, kocha Bernard Mwalala amesema “Tumepoteza lakini tumecheza vizuri sana kulinganisha tulivyocheza kwenye Kombe la shirikisho Afrika”.
Baada ya piga ni kupige kunako dakika 45 za mwanzo, kipindi cha pili Gor Mahia walitengeneza nafasi nyingi licha ya kushindwa kuzitumia mpaka dakika ya 63 ambapo Lawrence Juma aliifungia goli pekee Gor lililodumu mpaka kipenga cha mwisho cha mwamuzi.

Author: Bruce Amani

Share With Your Friends