Gor wapiga densi Cameroon hadi hatua ya makundi CAF

Sijui kule Cameroon wanacheza mtindo upi wa densi lakini ndivyo ilivyokuwa katika uwanja wa Omnisports mjini Limbe Jumapili ya leo Gor Mahia ilipolazimisha sare ya 0-0 dhidi ya wenyeji New Stars de Douala na kufuzu awamu ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Kogalo wanafuzu kwa jumla ya mabao 2-1 waliyosajili mkondo wa kwanza jijini Nairobi Jumapili iliyopita.

Hii inakua mara ya pili kwa mpigo Gor wanapenyeza awamu ya makundi baada ya msimu jana ambapo wamejihakikishia kitita cha Kshs 27 milioni.

Kwenye mtanange huu, kocha Hassan Oktay alikichezesha kikosi kilichoandikisha ushindi wa 2-1 mkondo wa kwanza uwanjani Kasarani.

Beki Philemon Otieno alikabidhiwa mikoba ya unahodha kwani beki Harun Shakava anatumikia adhabu ya kufungiwa mechi mbili waliyopewa na Shirikisho la Soka barani (CAF) pamoja na mwenzake Joash Onyango.

Droo ya makundi itafanyika hapo kesho Jumatatu mjini Cairo huku Kogalo wakitarajiwa kutua Dar es Salaam kwa michuano ya SportPesa Cup itakayong’oa nanga siku ya Jumanne.

“Tulifahamu mechi itakua ngumu kuliko mkumbo wa kwanza lakini nawashukuru vijana Wangu kwa kupambana hadi dakika ya mwisho,” kocha wa Gor Oktay alisema baada ya mechi.

Mwenzake Gerald Mbimi aliwalaumu nyota wake kwa kupoteza nafasi za wazi ambazo zingewapa goli moja tu ili kufuzu kwa mara ya kwanza makundi ya CAF.

“Tulikuwa na chakula mdomoni lakini tukajinyima kumeza sie wenyewe, sijui nisemeje kuhusu wachezaji Wangu maana tungemaliza mechi hii mapema sana,” alilia Mbimi.

Wachezaji wa New Stars walijigaragaza kwenye sakafu baada ya mwamuzi Kokou Ntale kutoka Togo kupuliza kipienga cha mwisho huku wenzao wakishangilia mbele ya mashabiki wa nyumbani.

Author: Bruce Amani

Share With Your Friends