Haaland awasha moto mechi ya kwanza Bundesliga, Dortmund wawakalia pabaya Bayern Munich

Kinda wa Borrusia Dortmund Erling Braut Haaland ameendeleza makali yake ya kufumania nyavu ambayo yalikuwa hayajaonekana kwa siku 70 kutokana na janga la virusi vya Corona ambalo limeshaitikisa Dunia.

Katika kandanda ya Bundesliga iliyopigwa leo kwenye dimba la Signal Iduna Park, Borussia Dortmund wameichapa Schalke 04 goli 4-0 huku kinda huyo akiandikisha rekodi ya kufunga goli la kwanza baada ya kabumbu kusimama kwa zaidi ya miezi miwili.

Mchezo huo utakumbukwa sana kutokana na hali yenyewe ilivyokuwa ukiwa kama mchezo wa watani wa jadi, lakini hakukuwa na shabiki hata mmoja tofauti na utamaduni ulivyokuwa awali, pia imeandikisha kuwa ligi ya kwanza kubwa barani Ulaya kurejea.

Kila kitu kilikuwa tofauti, wachezaji waliingia kwenye vyumba vya kubadilishia nguo kwa makundi, wachezaji waliingia uwanjani kwa gari tofauti tofauti, wachezaji wa akiba walikaa mita moja kutoka mchezaji mmoja kwenda mwingine huku wakivalia barakoa hata goli lilipofungwa hakukuwa na ushangilia wa pamoja.

Haaland alianza kuingia kambini dakika za mapema kupitia pasi murua ya Thorgen Hazard, kabla ya Raphael Guerreiro kufunga mawili na mchezaji aliyekuwa kwenye kiwango bora Thiago Hazard akafunga goli la mwisho linaloifanya Dortmund kufikisha pointi 54 alama moja kuifikia Bayern Munich ambayo ipo nafasi ya kwanza ambao wanacheza kesho Jumapili.

Katika matokeo mengine, RB Leipzig walikabwa kwa sare ya 1 – 1 na Freiburg huku Bertha Berlin wakiwafinya Hoffenheim 3 – 0. Wolfsburg waliwabwaga Augsburg 2 – 1 nao Paderdon wakatoka sare tasa na Duesseldorf.

Author: Bruce Amani

Share With Your Friends